IGP Sirro akaribishwa kwa mauaji Kibiti

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro akiwapa taarifa waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yake na wazee wa Mkoa wa Pwani katika mkutano uliofanyika jana wilayani Kibiti. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Wilaya za mkoani Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zimekuwa zikikumbwa na mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei mwaka jana na aliyeuawa juzi anakuwa mtu wa 32 kwa taarifa ambazo Mwananchi imekuwa ikizirekodi tangu mwaka jana.

Kibiti. Watu wasiojulikana juzi usiku waliua mkazi mwingine wa Ikwiriri, ikiwa ni saa chache kabla ya mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kutekeleza ahadi yake ya kukutana na wazee wa wilaya hizo za mkoani Pwani kuzungumzia visa hivyo.

Wilaya za mkoani Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zimekuwa zikikumbwa na mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei mwaka jana na aliyeuawa juzi anakuwa mtu wa 32 kwa taarifa ambazo Mwananchi imekuwa ikizirekodi tangu mwaka jana.

Mauaji mengi yamekuwa yakifanyika usiku kwenye nyumba za viongozi hao na watu wengine ambao wamewahi kushika uongozi, Idara ya Maliasili na askari wa Jeshi la Polisi. Kati ya watu hao, ni watatu tu ndio waliouawa na polisi baada ya kukataa amri ya kusimama.

Kamanda Sirro, ambaye aliapishwa wiki iliyopita kushika nafasi hiyo, aliitikia wito wa wazee wa wilaya hizo kutaka akutane nao na jana alikuwa anaanza mazungumzo hayo, lakini akakaribishwa na taarifa za kuuawa kwa askari wa mgambo aliyepigwa risasi nyumbani kwake.

Askari huyo, Erick Mwarabu alipigwa risasi tatu na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake, kitongoji cha Kazamoyo, Rufiji.

Mwarabu alivyouawa

Watu wa karibu na eneo hilo wamesema Mwarabu alipigwa risasi tatu na wauaji ambao walimtafuta na kumkuta akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda chake.

Iddy Malinda, mganga mkuu wa kituo cha Afya cha Ikwiriri, alisema amebaini majeraha matatu katika maeneo tofauti ya mwili wake.

“Mawili yalikuwa mbavuni upande wa kulia na moja kichwani,” alisema.

Alisema katika jeraha la kichwani, Mwarabu alipigwa risasi upande wa kushoto wa shingo yake iliyoharibu kichwa.

Alisema tayari mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Simon alisema watu hao walivunja mlango wa nyumba ya Mwarabu saa 9:00 usiku kisha kuingia ndani na kufanya mauaji hayo.

Simon alisema baada ya kuingia ndani, watu hao walipitiliza hadi chumbani kwake ambako walimkuta mke wake na kumshinikiza aeleze alipo Mwarabu.

“Walimpiga sana mke wake ili awaambie alipo mume wake, lakini hakuwaeleza wauaji alipo mume wake,” alisema.

Alisema baada ya kuona hataji alipo mumewe, walimtafuta ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kumkuta uvunguni mwa kitanda chake na ndipo walipompiga risasi akiwa uvunguni na baadaye kutoweka bila ya kuchukua kitu chochote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Tukio hilo limetokea wakati Kamanda Sirro akiwa anaanza mazungumzo na wazee kutafuta mbinu ya kuwakabili wauaji.

Juni 3, wazee wa Mkoa wa Pwani walimuomba IGP Sirro kwenda wilayani Kibiti ili azungumze nao kuhusu chanzo cha mauaji hayo ya mfululizo dhidi ya viongozi wa vijiji.

Siku moja baadaye, IGP Sirro alikubali wito huo na kueleza kuwa atakwenda wiki hii mara tu atakapopata ripoti ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Pwani.

Akizungumza na wazee hao jana, kamanda huyo wa zamani wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alisema mtenda maovu hulipwa maovu, hivyo wauaji hao watapatikana na malipo yao yatafanyika ndani ya muda mfupi.

“Pelekeni salamu kwa wauaji hao kwamba ubaya huwa unalipwa kwa ubaya siku zote. Pelekeni salamu kuwa siku zao zinahesabika,” alisema IGP Sirro katika kikao hicho kilichofanyika shule ya Sekondari Kibiti.

Hata hivyo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kushiriki katika mazungumzo hayo, badala yake IGP Sirro alizungumza nao baada ya kumaliza.

Sirro alisema mazungumzo kati yake na wazee wa wilaya za Kibiti na Rufiji yatafanikisha kuwakamata wauaji katika wilaya hizo.

Kiongozi huyo alisema wauaji hao hawatachukua muda mrefu kukamatwa na kuwataka wananchi kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake.

Aliwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pasipokuwa na hofu yoyote ile.

“Endeleeni kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi bila hofu yeyote, Serikali ipo nyuma yenu,” alisema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni aliyeambatana na IGP katika ziara hiyo alisema inasikitisha kuona watu wanauawa bila hatia hivyo kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwasaka wauaji hao kwa nguvu zote.

Masauni alisema usalama wa wananchi ni jukumu la wananchi wote, hivyo kuwataka kushirikiana na vyombo vya dola ili kuwakamata wahalifu wote.

Awali akifungua mkutano huo, mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamuhussein Kifu alisema tangu Aprili 30 mwaka jana hadi sasa watu 18 wakiwamo viongozi wa serikali za vijiji wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Kifu alisema miongoni mwa watu hao wamo viongozi wa vijiji, vitongoji, wanachama wa CCM na askari tisa.

Pia, Kifu alisema kibaya zaidi ni kuwa wengi wanaouawa ni wanachama wa CCM pekee na kutaka mauaji hayo yakomeshwe.

Mmoja wa wazee waliohudhuria mkutano huo, Mohammed Issa alisema mazungumzo hayo yamekuwa na tija na yametoa mwanga wa kukomesha mauaji hayo.

Alisema wazee watahakikisha wanashirikiana na IGP Sirro hadi kukomesha mauaji hayo.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM wilayani Kibiti, Musa Mnyelesa alisema hakuna haja ya kutumia nguvu katika sakata hilo la mauaji mfululizo na kuisifu hatua ya IGP Sirro kuzungumza na wazee hao.

“Kutumia nguvu kunawajenga hofu wananchi. Wanahitaji kupata nafasi ya kuhojiwa kistaarabu na hatua ya Sirro inaweza kufanikisha kupata suluhisho,” alisema.